Baadhi ya vijana kutoka Nyamira kaskazini wamekitaka chama cha ODM kuwafukuza chamani wanachama wanaokiuka sheria na masharti ya chama.
Wakihutubu kwenye hafla ya mazishi kule Ikonge siku ya Jumapili, vijana hao ambao ni wafuasi sugu wa chama cha ODM walisema kwamba wanachama wa aina hiyo wanazuia ukuaji wa chama hicho mashinani, huku wakilaumu usimamizi wa chama hicho kwa kushindwa kuwathibiti wanachama wanaopinga sera za chama.
“Sisi kama vijana wafuasi wa chama cha ODM kwa kweli hatujafurahishwa na jinsi usimamizi wa chama cha ODM unavyoshughulikia swala hili la baadhi ya wanachama kukiuka sera na sheria za chama,” alisema msemaji wao Dominic Ombonyi.
“Wakati umefika kwa baadhi ya maafisa chamani kujiuzulu kwa kuwa hatuwezi tukaketi na kuangalia wanachama wa ODM wakiuza sera za vyama pinzani,” aliongeza Ombonyi.
Vijana hao aidha walikipa chama hicho makataa ya mwezi mmoja kuwaadhibu wanachama wanaokiuka masharti ya chama, la sivyo wafanye maandamano huku wakitaka maafisa wakuu wa chama kujiuzulu iwapo watakosa kuwachukulia hatua wanachama husika.
“ODM ni chama cha wananchi, na yeyote anayefikiria hawezi akatii sheria za chama sharti ajiuzulu ili aruhusu uchaguzi mpya kufanywa, na inastahili usimamizi wa chama ujiondoe afisini iwapo hawatowachukulia hatua za kisheria watu wa aina hiyo,” aliongezea Ombonyi.