Share news tips with us here at Hivisasa

Mashabiki wa mwanamziki maarufu nchini Diana Chemutai Rono maarufu kama Chelele mjini Nakuru, wameeleza kusikitishwa na kifo chake, wakitaka uchunguzi kufanyika kuhusu kifo chake tatanishi.

Mwili wa Chelele aliyetunga nyimbo maarufu kama Binti Osama, ulipatikana kwenye veranda ya nyumba yake iliyopo eneo la Kapwen, kaunti ya Bomet Jumamosi asubuhi.

Kamanda wa polisi katika kaunti hiyo Leah Kithei alisema kwamba mwili wa marehemu mwimbaji huyo ulikuwa na majeraha kadhaa ya kudungwa, na kuna vidokezo kwamba aliuliwa kwingineko na kisha mwili wake ukatupwa nyumbani kwake.

Mfuasi wake mmoja mjini Nakuru na mpenzi wa nyimbo zake Jane Chebet, amesema kwamba kifo cha Chelele ni pigo kubwa kwake kwani hangekosa kuhudhuria tamasha zozote za nyimbo alizokuwa akiandaa marehemu.

Naye Stephen Kiprop, alisema inahuzunisha kuona maisha ya mwanamziki huyo mchanga yakitamatika katika njia isiyoeleweka, miezi michache baada yake kunywa sumu na kulazwa hospitalini.

“Tumepoteza kama Wakenya, na jamii ya Wakalenjin mwanamziki aliyevutia kwa nyimbo tamu na zilizodhihirisha utamaduni wetu,” alisema Wisley Taalam.

Chelele ameacha watoto wawili mapacha.