Share news tips with us here at Hivisasa

Wafuasi wa chama cha Vugu vugu la Maendeleo Chap Chap Movement lililozinduliwa na Gavana wa kaunti ya Machakos katika eneo la Changamwe kaunti ya Mombasa, wamebaki na mshangao baada ya watu wasiojulikana kufuta jina la ofisi yao katika hali ya kutatanisha.

Faustine Mwanzia Makenga mmoja wa maafisa wakuu wa vuguvugu hilo ameikashfu vikali kitendo hicho na kuwaonya vijana kujiepusha na watu wasiopenda maendeleo kwani hatua hiyo huenda ikachangia uhasama na kusababisha vurugu.

Akizungumza na wanahabari nje ya ofisi hiyo huko Changamwe mjini Mombasa siku ya Jumanne, Makanga amesema kuwa watahakikisha kuwa vijana wanadumisha amani na suala la maendeleo katika eneo hilo linatekelezwa na viongozi waadilifu na wenye azma ya kubadili uongozi wa nchi.

“Tumesikitishwa na hatua hii na tunawaambia wale mahasidi wetu kuwa chama chetu kitaendelea na kuwa na ofisi hapa na tutahakikisha chama hiki kina wafuasi kama vyema vyengine, hii ni nchi ya demokrasia kwa hivyo tuko na haki kikatiba kuwa na chama," alieleza Makanga.

Naye Patricia Mutheu ambaye ni mjumbe katika chama cha TNA eneo la Changamwe amewataka wakazi kutokubali kutumiwa vibaya na viongozi na badala yake kuheshimu maamuzi ya kila Mkenya kwa kuzingatia uhuru wa demokrasia na kutetea chama.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Gavana wa kaunti ya Machakos Alfred Mutua kuzindua rasmi ofisi ya vuguvugu hilo huko changamwe, lengo kuu likiwa kuleta maendeleo karibu na mwananchi mashinani.