Baadhi ya wafugaji wa ng'ombe wa maziwa kutoka eneo bunge la Borabu wamepata sababu ya kutabasamu baada ya mbunge wa eneo hilo kuchimba visima vya maji vitakavyosaidia mifugo yao kupata majikwa urahisi hasa wakati wa msimu wa ukame.
Wakiongozwa na Vincent Momanyi, wakulima hao walisema kuwa mradi huo wa visima utawasaidia pakubwa kuimarisha uzalishaji wa maziwa miongoni mwa ng'ombe za maziwa.
"Watu wengi katika eneo hili ni wafugaji wa ng'ombe wa maziwa na wanaotegemea pakubwa kupata riziki yao kutokana na uuzaji wa maziwa na visima hivi ni vya umuhimu mkubwa kwa maana vitatuwezesha kupata maji ya kunywa kwa mifugo yetu hasa wakati wa msimu wa ukame," alisema Momanyi.
Wakulima hao aidha walichangamkia suala la ukarabati wa vyogesho kumi vya mifugo wakisema kuwa hali hiyo itasaidia pakubwa kupunguza mzigo wa kutibu mifugo kila mwezi.
Aidha, waliipa changamoto serikali ya kaunti hiyo kuanzisha kiwanda cha maziwa ili kupunguza visa ambapo baadhi ya wakulima hulazimika kupeleka maziwa yao hadi Bomet.
"Tumekuwa tukizikosa huduma za vituo vya kuosha ng'ombe kwa zaidi ya miongo miwili ila ni furaha yetu kwamba baadhi ya vituo hivyo vimekarabatiwa ila changamoto sasa ni kwa serikali kuhakikisha kuwa inajenga kiwanda cha maziwa huku Nyamira," aliongezea Momanyi.
Mradi huo uliogharimu shillingi millioni 10 ulitekeleza kwenye wadi ya Nyansiongo, Mekenene na Esise.
Ngombe za maziwa. Wafugaji wa eneo la Borabu wana kila sababu ya kutabasamu huku mbunge wa eneo hilo akiwachimbia visima.