Wafungwa katika gereza la Naivasha wanawataka wabunge watupilie mbali hukumu ya maisha pamoja na ile ya kunyongwa.
Wakiongea siku ya Jumatatu na kamati ya bunge kuhusu maswala ya wafungwa, walisema hukumu hizo mbili zinazidi kutesa washtakiwa wengi ambao tayari wamebadilisha mienendo yao.
Aidha wafungwa kwenye gereza hilo walisema wengi wao kwa sasa wametubu dhabi zao na wanashiriki masomo. Kuwachiliwa kwao, walisema, kutafaidi jamii kwani wamepata ujuzi katika Nyanja mbalimbali wakati wa vifungo vyao.
“Hukumu ya maisha na kunyongwa inamaanisha utasalia kizuizini licha ya kuwa umebadilika. Hilo linaumiza wengi wetu hapa,” John Kamau alisema.
Wanachama wa kamati hiyo inayooongozwa na mbunge Grace Kiptui waliahidi wafungwa hao kuwa bunge itashughulikia swala hilo.