Wafungwa wanaotumikia kifungo katika gereza la Shimo la Tewa jijini Mombasa wametoa wito kwa kamati ya msamaha kwa wafungwa kusamehe wafungwa waliotumikia zaidi ya miaka 15 gerezani na kuwaachilia huru.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatano katika gereza hilo kwa niaba ya wafungwa wenzake katika gereza la Shimo la Tewa, George Mungai alisema kuwa kutolewa kwa msamaha huo kunatoa matumaini kwa wafungwa wengine waliomo gerezani haswa baada ya kupitia marekebisho ya tabia wakiwa gerezani humo.
Mungai aliongeza kuwa wafungwa wengi hupoteza matumaini ya kuachiliwa huru pindi wanapoingia gerezani humo na kukutana na wenzao waliotumikia miaka mingi akisema kuwa msamaha unaotolewa utasaidia pakubwa katika kupunguza idadi ya wafungwa walioko katika gereza za humu nchini.
Kwa upande wake naibu mwenyekiti wa kamati hiyo Regina Saira Boisabi alisema kuwa kufikia sasa wameshazuru zaidi ya magereza 70 humu nchini ili kuwahamasisha wafungwa kuhusiana na majukumu ya kamati hiyo kutokana na wafungwa wengi kutokuwa na ufahamu wa kamati hiyo iliyoasisiwa kwa mujibu wa katiba ya mwaka 2010.
Kulingana mkuu wa gereza hilo upande wa wanawake Leah Mukora, kuna wafungwa wa kike 241 pamoja na watoto 18 wanaoishi na mama zao katika gereza hilo.
Mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi katika gereza hilo ni miaka sitini ambaye anatumikia kifungo baada ya kupatikana na kosa la mauaji.
Haya yalizungumzwa wakati wa sherehe ya kuwakabidhi zawadi za kufunga mwaka wafungwa wa kike katika gereza hilo, kupitia ufadhili wa kamati hiyo ambapo watoto hao pia wametunukiwa zawadi.