Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Naibu Kamishna wa Kaunti ndogo ya Kisauni Julius Kavita amesema kwamba agizo lililotolewa na Kamishna wa kaunti Nelson Marwa la kulikabili barabara kundi la wahalifu la 'Wakali Kwanza' na 'Wakali Wao' litatekelezwa kikamilifu.

Akizungumza na wanahabari katika eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Kavita alisema kwamba inasikitisha sana kuona vijana wadogo wakijitosa katika uhalifu wakisalia kimya badala ya kuwaripoti kwa maafisa wa polisi.

Aidha aliongeza kwamba washukiwa watatiwa nguvuni na kuzuiliwa na maafisa wa polisi kabla ya kufunguliwa mashtaka mahakamani, huku akihoji kwamba ni lazima wazazi wa eneo hilo wayawajibikie majukumu yao kikamilifu.

Akikiri kwamba maeneo ya Mishomoroni, Bamburi, Mtopanga, Mwandoni na Barsheba yanashuhudia mchipuko wa makundi ya kihalifu na ambayo yamewalenga wakazi wanaorauka katika shughuli zao na lazima makundi hayo yataangamizwa.

“Agizo lililotolewa na Kamishna wa kaunti hii lazima litekelezwa kikamilifu ili kuwasaidia wakazi kutohangaishwa na kuporwa mali zao na baadhi tu ya makundi ya kihalifu,” alisema Kavita.

Kauli ya Kavita inajiri baada ya Kamishna Marwa kusema kwamba ataongeza maafisa wa Polisi katika kuwakabili vijana waliyojitosa katika makundi ya kihalifu kaunti ya Mombasa.