Wahudumu wa tuktuk katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa wametishia kufanya maandamano ikiwa bado unyanyasaji barabarani utaendelea.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Alhamisi wakiongozwa na Karama Mwamburi, wahudumu hao walidai kuwa maafisa wa trafiki huwatoza ada zisizo halali na ambazo ni ghali kupindukia.

"Waweza ukatozwa hadi shilingi elfu tatu ukikamatwa kwa kosa la kubeba abiria wengi au hata ukiwa huna vibali vinavyotakikana. Mara nyingine watoa pesa hata kama huna kosa," alisema Mwamburi.

Wahudumu hao hata hivyo wamesema kuwa iwapo masaibu yao hayatashughulikiwa, wataandamana kushinikiza mabadiliko.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya wenzao mjini Mombasa kufanya maandamano hadi jengo la bunge la kaunti.