Huenda wakazi wa Kaunti ya Nyamira ambao kwa muda sasa wamekuwa na changamoto za kupokea huduma za afya kwenye hospitali mbalimbali kutokana na upungufu wa wahudumu wa afya  wakapata sababu baada ya serikali ya kaunti hiyo kuajiri zaidi ya wahudumu 220 wa afya. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Akihutubu kwenye shule ya upili ya Kebirigo, kule Nyamira siku ya Jumatano wakati wa kuwapa mafunzo wahudumu hao kabla ya kuripoti kwenye vituo vya kazi, katibu wa afya kwenye kaunti hiyo Douglas Bosire aliwahimiza wafanyikazi hao kuwahudumia wananchi bila ubaguzi na kutojihuzisha na wizi wa dawa na vifaa vya hospitali. 

"Ni himizo langu kwenu wahudumu wa afya kuhakikisha kuwa mnawahudumia wananchi bila ubaguzi na kwa kweli itakuwa vibaya kusikia kuwa mmejihusisha na masuala ya wizi wa dawa  na vifaa vya hospitali kwa kuwa hilo kamwe halitaruhusiwa hapa Nyamira," alisema Bosire. 

Katibu huyo aidha alihoji idara ya afya ina upungufu wa wahudumu wa afya, ila aliyasihi mashirika yasiyo ya serikali kuajiri wahudumu zaidi wa afya kwa minajili ya kusaidia kaunti hiyo kukabili upungufu wa wahudumu wa afya. 

"Kwa kweli idara ya afya ina upungufu mkubwa wa wahudumu, ila ni ombi langu kwa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kuajiri wahudumu kwa njia za kandarasi ili watusaidie kukabili changamoto hii," aliongezea Bosire.