Wahudumu wa pikipiki pamoja na baiskeli wamelalamikia kuitishwa hongo kutoka kwa askari wa kampuni ya kibinafsi ya kuweka usalama katika kivuko cha feri cha Likoni katika Kaunti ya Mombasa.
Wakazi hao wanasema kuwa askari wa kampuni hiyo huwashika kwa kuwasingizia kwa makosa ambayo hawajafanya, na kuwatishia kuwapeleka kwenye kituo cha polisi iwapo hawatatoa 'kitu kidogo' wawachilie, hali ambayo wanasema inafanyika kila mara.
Kulingana na Samson Tenai, ambaye alikuwa akiongea siku ya Jumatatu wakati wakimtoa mwenzao ambaye alishikwa kwa madai ya kuvunja sheria, wamejaribu kuwaelezea wasimamizi swala hilo, lakini hatua huchukuliwa na hudumu kwa muda na ata wakati mwingine wanatakiwa kutoa ushahidi wa kuthibitisha madai kama hayo.
“Hamna mtu ambaye anashughulikia swala hilo likapata suluhu, kwa sababu mara nyingi tunaambiwa kutoa ushahidi ambao inakuwa vigumu kuwa nao, na ukionekana kuwasema watakuonea kila mara unapokuwa unavuka kwenye kivuko hicho,” alisema Tenai.
Wakazi hao wameitaka serikali ya kaunti kwa ushirikianao na mamlaka ya shirika la feri nchini kuangalia na kuchunguza malalamishi hayo, na kusema kuwa wengi wao ni vijana wa kujitegemea na hutumia baiskeli hizo kubebea bidhaa zao kutoka soko kuu la Kongowea.
Hata hivyo, baadhi ya askari ambao tuliozungumza nao walikana madai hayo, na kusema kuwa wao hufuata sheria wanapotekeleza shughuli zao kwenye kivuko hicho.