Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wahudumu wa bodaboda eneo la Ahero wametakiwa kufunga kazi yao mwendo wa saa tatu usiku, ili kuruhusu polisi kufanya doria kukabiliana na wezi walio na bunduki ambao wanahangaisha wakazi wa Ahero, Bahati na Maili Kumi.

Akiongea katika mkutano uliowaleta pamoja wanabiashara wa maduka, wana boda boda na vijana wanaofanya kazi kwenye karakana za eneo la Ahero kwenye uwanja wa kanisa la PCEA, naibu kamishna katika kaunti ndogo ya Bahati Kithinji Ithai alisema wahalifu hawabagui yeyote, akirejelea kisa ambapo yeye alivamiwa kati kati ya mji wa Nakuru mwaka wa 2010 na wezi waliopora bidhaa zake kwenye gari.

“Wezi wanaovamia wakazi hapa kwa bunduki sio wenyeji, lakini huja kufanya upelelezi kwanza kwa ushirikiano na baadhi yenu hatimaye wanatekeleza uhalifu. Kama usalama utaimarika, utaimarishwa kupitia ushirikiano wenu,” alisema Ithai. 

Aidha aliwataka kupiga ripoti kwa kutuma ujumbe mfupi kwa nambari 22068.

Chifu mkuu wa eneo hilo Paul Mbuthia naye aliwataka wananchi kuripoti visa au yeyote wanayemshuku, ambapo pia alichangamoto wanabiashara kuajiri walinzi wa kulinda biashara zao nyakati za usiku.

Mkutano huo ulifanyika baada ya wezi waliokuwa na bunduki kuvamia mwanabiashara mmoja eneo hilo nyumbani kwake usiku wa Jumanne, lakini ushirikiano wa polisi na raia ukafanikiwa kutibua njama hiyo.

Chifu Mbuthia aliwataka wakaazi hao kutilia mkazo mpango wa nyumba kumi akisema utapunguza wizi kwa aslimia 80.

“Kama hatujuani hatuwezi kupigana na uhalifu. mjue mwenzako kwa sababu usalama unaanza na mtu binafsi,” alisema Mbuthia.