Wahudumu wa matatu mjini Kisii wametishia kususia kulipa ushuru, kwa kutokarabatiwa kwa kituo chao cha magari mjini humo jinsi gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae aliahidi hapo mbeleni.
Kulingana na wahudumu hao, Gavana Ongwae na naibu wake Joash Maangi walipotembelea kituo hicho waliahidi wahudumu hao wa matatu kuwa kituo chao kingekarabatiwa kikamilifu, na kujenga vibanda vya abiria kupumzikia, jambo ambalo halijazaa matunda kwa mda mrefu sasa.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne katika kituo hicho mjini Kisii, wahudumu hao, wakiongozwa na mwenyekiti wa chama cha wahudumu wa matatu Okong’o Mose walisema kituo hicho hakijakarabatiwa kikamilifu, ukosefu wa vyoo vya wahudumu hao, mazingira mabaya na mengine mengi, huku akisema huenda wahudumu hao wasusie kulipa ushuru kwa kutotimiziwa ahadi walizopewa hapo mbeleni.
“Katika kituo hiki chetu cha magari, hakuna vibanda penye abiria wetu wanaweza kupumzikia, mazingira mabaya kwani uchafu hautolewi kwa wakati ufaao, ingawa wa kufanya usafi mjini humu wako, hakuna vyoo na mengine mengi,” alisema Mose.
“Tunaomba gavana Ongwae atimize ahadi alizotoa alipotembelea kituo hiki akiwa na naibu wake Joash Maangi ili ushuru ule tunakata itumike kutufanyia yale tunahitaji,” aliongezea Mose.