Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku sherehe za krismasi na mwaka mpya zikiwadia, wahudumu wa tuk tuk katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kuwa waangalifu ili kuzuia kushuhudiwa kwa ajali barabarani.

Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, mwenyekiti wa chama tuk tuk kaunti ya Mombasa Obedi Miruli alisema kwamba mwezi huu wa Desemba mji wa Mombasa hushuhudia ongezeko la watu kutoka sehemu mbali mbali za nchi wanaozuru kujivinjari, na akawasihi wahudumu hao kuwa waangalifu zaidi barabarani.

Aidha amesema kwamba kwa kuzingitia sheria za trafiki, ajali nyingi katika kaunti hiyo zitapungua kwa asilimia kubwa, huku akiwatahadharisha wahudumu hao kuwa waangalifu dhidi ya kuwabeba wahalifu walio tishio kwa wageni.

"Ni lazima kwa wahudumu wa tuk tuk kuwa waangalifu hasa wakati huu tunapoelekea kwa shamrashamra za sherehe za krismas na mwaka mpya ili kupunguza idadi ya ajali za barabarani," alisema Miruli.

Wakati uo huo, amewataka maafisa wa polisi pamoja na maaskari wa Kaunti ya Mombasa kutowahangaisha wahudumu hao wa tuk tuk katika msimu huu wa shamra shamra za sherehe za krismas na mwaka mwapya ili kufanikisha shughuli za uchukuzi.

"Tunawaomba pia maafisa wa polisi na wa kaunti ya Mombasa kushiriana na wahudumu wa tuk tuk vyema na kusitisha kuwahangaisha ili nao wajitafutie riziki msimu huu," aliongeza Miruli.