Sakata ya kufujwa kwa milioni 791 za shirika la huduma za vijana kwa taifa NYS imechukua mwelekeo mpya baada ya aliyekuwa waziri wa ugatuzi Bi Ann Waiguru kuwahusisha viongozi wakuu serikalini kwenye sakata hiyo ya wizi wa mamilioni ya fedha.
Viongozi hao ni pamoja na kiongozi wa walio wengi bungeni ambaye pia ni mbunge wa Garissa mjini Bwana Aden Duale, naibu kiongozi wa wengi katika bunge la seneti Kipchumba Murkomen na msaidizi wa naibu rais Farouk Kibet.
Katika hati ya kiapo aliyowasilisha mahakamani, Waiguru amemlaumu pakubwa seneta Kipchumba Murkomen kwa masaibu yanayomkabili kwa usemi kuwa seneta huyo alimtishia kuwa endapo hatasitisha uchunguzi kuhusu kupotea kwa shilingi milioni 791 za NYS angepanga njama ya kumpaka tope.
"Mwezi Julai seneta Murkomen alinitembelea afisini na kuniarifu kwamba ametumwa na wateja wake waje kiniambia nitafute mbinu ya kusitisha uchunguzi wa sakata ya NYS na iwapo sitafanya hivyo nitajutia," alisema Waiguru.
Waiguru pia amesema kuwa Farouk Kibet alihusiana kwa karibu na mfanyibiashara Ben Gethi, Peter Mang'iti na Nelson Githinji ambao ni washukiwa wakuu kwenye sakata hiyo na pia alipokea kiasi cha pesa hizo za NYS.
"Wakati wa uchunguzi wa sakata ya NYS kulikuwa na mawasiliano ya karibu kati ya Ben Gethi na aliyekuwa kiongozi wa NYS Nelson Githinji na Peter Mangiti," alisema Waiguru.
Waiguru aliongeza kuwa Aden Duale alimuandikia ujumbe mkurugenzi wa NYS Adan Harakhe wakati wa uchunguzi wa sakata ya NYS na kumtahadharisha kuwa kuteuliwa kwake kunategemea hatma ya chama cha URP kwani viongozi kutoka eneo lake wako chini ya chama hicho, kwa hivyo awe makini ama aondolewe afisini.
Waiguru aidha amekana kuhujumu uchunguzi wowote wa NYS au kukutana na mfanyibiashara Josphene Kabura.