Share news tips with us here at Hivisasa

Kiongozi wa wanawake wa jamii ya Kalenjin katika eneo la Solai amemtaka aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Bi Ann Waiguru, kuandikisha ripoti kwa polisi kuhusiana na vitisho ambavyo amekuwa akipokea kutoka kwa viongozi mbalimbali serikalini baada yake kuwataja katika sakata ya shirika la NYS.

Akizungumza na wanahabari siku ya Jumanne, Gladys Keter alisema kuwa ripoti hiyo itamsaidia Waiguru iwapo chochote kitamtendekea.

“Hivi maajuzi tulimsikia kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale akisema kuwa ‘atapambana na Ann Waiguru’ na matamshi kama hayo huwezi jua hatma yake. Ikiwa umetajwa kuwa ulihusika na ufisadi, unapaswa ujitokeze kwa ustaarabu na udhihirishe kuwa hukusika. Vitisho havitakusaidia,” alisema Bi Keter.

Kiongozi huyo ameitaka serikali kumpa waziri huyo wa zamani wa ugatuzi ulinzi wa kutosha kwa kusema kuwa ripoti aliyoandikisha ndiyo itakayopeleke kushtakiwa kwa wote waliohusika katika sakata nzima ya NYS.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya Bi Ann Waiguru kudai kuwa maisha yake yamo hatarini.

Kupitia barua yake kwa Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet, Bi Waiguru alitaka kupewa ulinzi huku akisema kuwa amekuwa akipokea vitisho tangu alipowataja Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale, Naibu wa Kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen, Waziri wa Fedha Henry Rotich na msaidizi wa Naibu wa Rais William Ruto Farouk Kibet kuhusika katika sakata ya NYS.