Wakaazi Kisii wameikosoa serikali ya kaunti hiyo, kwa kusimamisha shughuli ya kueleza jinsi wamekuwa wakitumia pesa, haswa katika maendeleo.
Hii ni baada ya spika wa bunge la kaunti ya Kisii Okerosi Ondieki, na wawakilishi wadi wa kaunti hiyo, kuagiza waziri wa fedha Kodek Omwancha, kueleza jinsi pesa hizo zimetumika, huku wakidai kuwa zilikuwa zikitumiwa vibaya.
Wakaazi wa kaunti hiyo pamoja na waandishi wa habari, waliarikwa kwa shughuli hiyo ili kujua jinsi pesa zilikuwa zikitumika lakini spika Ondieki aliahirisha shughuli hiyo hadi siku ya Jumatatu mapema wiki hii.
Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano mjini Kisii, wakaazi hao wakiongozwa na Haron Moreka na Samuel Makombi, walikosoa serikali ya kaunti hiyo kwa kusimamisha shughuli hiyo wakidai kuwa huenda shughuli hiyo imekomeshwa ili kuficha yaliyokuwa yakiendelea katika serikali hiyo.
“Tumeshangaa ni kwa nini shughuli hiyo imesimamishwa ghafla hata baada ya kualikwa,” alisema Moreka.
Ripoti iliyowasilishwa katika bunge hilo, ilionyesha kuwa mamilioni ya pesa yalitumika kwa miradi ambayo haijulikani, jambo ambalo liliwalazimu wawakilishi; Francis Aburi na Timoty Nyarang’o kuhoji jinsi pesa hizo zilitumika.