Share news tips with us here at Hivisasa

Wakaazi wa kaunti ya Nakuru wametakiwa kuwa makini ili kuepuka kutapeliwa na polisi bandia.

Wito huo ulitolewa na OCS wa kituo cha polisi cha Bondeni kilicho viungani wa mji wa Nakuru Pascal M Kiamba, kufuatia hatua ya kukamatwa kwa mwaname mmoja mwenye umri wa makamo ambaye amekuwa akiwahangaisha wahudumu wa pikipiki na kuwaitisha hongo akijifanya afisa wa polisi.

Akizungumza Jumamosi aliwataka wananchi pia kuwa macho ili kujiepusha na matapeli wanaojidai kuwa maafisa wa polisi huku akisema ni wajibu wa kila mwananchi kuwasaidia polisi kunasa matapeli hao.

Pamoja na hayo, amewaonya wakaazi wa Nakuru dhidi ya kuwafungulie watu wanaojidai kuwa maafisa wa polisi milango yao haswa wakati wa usiku akisema idara ya polisi imetoa nambari ambayo wananchi wanaweza kupiga ili waweze kubaini iwapo watu hao ni maafisa wa polisi au ni walaghai.

Kulingana naye, baadhi ya njia za kutambua iwapo afisa wa polisi ni halali ni kupitia sare rasmi za polisi na gari la polisi linalofaa kuwa na rangi kamili pamoja na nambari za usajili za polisi.