Wakaazi wa Mombasa wameutaja uongozi mbaya na kukosa mpangilio bora wa kuunda tume za kuchunguza utumizi mbaya wa fedha za umma kama sababu ya kukithiri kwa ufisadi nchini.
Katika mahojiano na mwandishi huyu siku ya Ijumaa, baadhi ya wakaazi wa Mombasa waliwalaumu viongozi kwa kupokea hongo katika kuhudumia mwananchi, huku wakiunga ripoti ya kimataifa kuwa taifa la Kenya lina ufisadi mwingi.
Wakingozwa na Helen Kilonzi, wakaazi hao walidai kuwa utaratibu unaotumiwa kuwachagua maafisa hao umejikita katika misingi ya ufisadi hivyo kuwa vigumu kumaliza ufisadi hapa nchini.
Kauli hii inajiri baada ya taifa la Kenya kuorodheshwa miongoni mwa mataifa yaliyo na ufisadi wa kupindukia ulimwenguni.
Kulingana na ripoti ya shirika la Transparency International, taifa la Kenya ni nambari 139 kati ya mataifa 168 yaliyo na ufisadi wa juu.