Wakaazi wa Kaunti ya Mombasa wamemtaka Seneta Hassan Omar kuendelea kuwa seneta na kuacha siasa za mapema.
Wakiongea na mwandishi huyu jijini Mombasa siku ya Jumatatu, wakaazi hao walisema kuwa ni mapema kwa viongozi hao kuanza kuonyesha tofauti zao na sharti watimize ahadi walizotoa kwa wananchi kabla ya kuanza kupimana nguvu kisiasa.
Akiongea kwa niaba yao mchanganuzi wa masuala ya kisiasa kwenye bunge la raia Samora Mwehu, alishangaa kwa nini Seneta Omar ameanza kuonyesha tofauti ilhali kuna mengi bado amebakisha kutimiza tangu kuanza hatamu yake ya useneta.
Mwehu alisema ni vigumu kwa wakaazi hao kuamua ni nani ambaye atapewa nafasi hiyo ikizingatiwa kuwa kuna viongozi wengi wa kisiasa ambao tayari wameonyesha nia ya kumpinga gavana wa sasa Hassan Joho.
“Hatuko tayari kuwekwa katika vipimo vya siasa huku wanasiasa hao hawajafanikisha ahadi walizowapa wapiga kura wakati wa kutafuta kura zao. Tunawaambia peupe kuwa hatupo tayari kamwe kuingia siasani kwa sasa,” alisema Mhemu.
Aliongeza, “Lazima watimize yote na seneta wetu Omar ajue alituahidi mengi kama haki za msingi za wakaazi ambao wamedhulumiwa kwa muda mrefu.”