Huku shamra shamra za sikukuu ya mwaka mpya zikizidi kung’oga, wakazi wa kaunti ya Mombasa wameshauri kuwa waangalifu dhidi ya wahalifu wanaolenga kuvuruga usalama wa kaunti hiyo.
Afisa wa kitengo cha dhararu wa Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini Muhuri, Fahad Changi amesema kuwa mara nyingi wahalifu hutumia fursa ya kutekelezwa uhalifu mahali panapokuwa na wakaazi wengi wakijivinjari na akawataka kuwa katika mstari wa mbele kutoa habari muhimu kuhusu washukiwa wa uhalifu ili kutiwa nguvuni.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Afisa huyo wa kitengo cha dhararu katika shirika hilo, amehoji kuwa iwapo wakaazi watashirikiana vyema na maafisa wa usalama basi visa vyingi vya kihalifu vitasitishwa kwa kiwango kikubwa na usalama wa eneo hilo utaimarika.
"Tunawatahadharisha wakaazi kuwa waangalifu dhidi ya wahalifu hasa wakati huu wa shamra shamra za sherehe za mwaka mpya kwa sababu wahalifu wengi hupenda kutumia fursa hiyo kutekeleza uhalifu", alisema Changi.
Wakati uo huo amewataka maafisa wa usalama kutodharau taarifa zinazowasilishwa na wakaazi kwao kuhusu washukiwa wa uhalifu ili kuona kwamba swala zima la usalama linachukuliwa kwa uzito.
"Tunawauliza maafisa wa usalama kushika doria kikamilifu ili kuhakikisha kuwa usalama wa eneo hili uko salama," aliongeza mwanaharakati huyo wa kijamii.
Kauli ya mwanaharakati huyo imejiri siku chache tu baada ya idara ya usalama kaunti ya Mombasa kuwatia nguvuni washukiwa watatu wa ugaidi wanaodaiwa kupanga njama ya kutekeleza mashambulizi katika kaunti hiyo.