Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi mjini Nakuru wametoa maoni tofauti kuhusiana na pendekezo la kuhalalishwa kwa ukahaba mjini humo.

Wakizungumzia pendekezo la mbunge wa Nakuru mjini magharibi Samwel Arama, aliyetaka ukahaba uhalalishwe, wakaazi wengi wamepinga pendekezo hilo huku wengi wakiliunga mkono.

Janet Kanini ambaye ni mfanyibiashara na mkristo amesema kuwa jamii na mila ya kiafrika haikubalii ukahaba na kuwa itakuwa makosa kuuhalalisha.

“Inasikitisha kuwa tabia hii ya ukahaba imekithiri hapa kwetu na ni dhahiri kwamba jamii imeharibika lakini hatuwezi kubali tabia hiyo mbaya ihalalishwe kwa sababu watoto wetu wataharibika,” alisema Kanini.

Timothy Gatobu ambaye ni mhadhiri wa somo la dini katika chuo kikuuu kimoja Nakuru amesema kuwa kuhalalisha ukahaba itakuwa sawa na kuhalalisha maovu katika jamii.

“Kama tutahalalisha ukahaba basi tutakuwa tunafungua mlango kwa maovu mengi kwa sababu hata wezi watataka wizi uhalalishwe na hiyo sio njia nzuri kufuata,” alisema Gatobu.

Mary Mwende ambaye ni mwanafunzi wa chuo kikuu analiunga mkono pendekezo hilo na kusema kuwa litasaidia kumaliza mauaji ya makahaba na pia serikali itafaidika kwa kukusanya ushuru.

“Ukahaba ni kama biashara nyingine na mimi sioni kama ni makosa wakikubaliwa kufanya kazi yao bila kusumbiliwa na polisi na pia itasaidia serikali kwa sabau watapata ushuru kutoka kwa makahaba,” alisema.

Jumapili iliyopita Arama alitoa pendekezo hilo la kuhalalisha ukahaba kama njia moja ya kumaliza mauaji ya makahaba mjini Nakuru.