Kufuatia visa vya uhalifu na jaribio la ugaidi kuendelea kuripotiwa katika maeneo mengi nchini, Gavana wa Kaunti ya Nyamira John Nyagarama amewasihi wakazi wa kaunti kuwa macho hasa msimu huu wa sherehe za krismasi.
Akihutubu kwenye hafla ya kuchangisha pesa za ujenzi wa kanisa la PAG kule Matutu siku ya Jumapili, Gavana Nyagarama alisema kuwa hakikisho la usalama ni jukumu la kila mwananchi.
Alisema kuwa yafaa wananchi washirikiane kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa miongoni mwao.
"Sharti kila mmoja wetu ahakikishe kuwa usalama unadumishwa miongoni mwetu na sharti tuwe tayari kupeana ripoti kwa maafisa wa polisi ili ikiwa kuna watu tunaowashuku kuwa tishio kwa usalama wetu, waweze kukabiliwa," alisema Nyagarama.
Nyagarama aidha alisema kuwa serikali yake itashirikiana na ile ya kitaifa ili kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa miongoni mwa wakazi wa kaunti hiyo.
"Serikali yangu imeweka mikakati kuhakikisha kuwa tunashirikiana kikamilifu na serikali ya kitaifa ili kuwahakikishia wananchi usalama wao. Tayari kamishna Onung'a amesema amethibitisha kuwa maafisa wa polisi watakuwa wakiweka doria hasa majira ya usiku kama njia mojawapo yakuimarisha usalama," alisema Nyagarama.