Wakaazi wa eneo bunge la Bahati wamewalaumu maafisa wa usalama kwa madai ya kuzembea kazini na hivyo kufanya wahalifu kuhangaisha wakaazi.
Wakikashifu mauaji ya mwanabiashara mashuhuri katika eneo hilo aliyeuawa kwa kupigwa risasi, wakaazi hao wamesema maafisa wa polisi kwenye kambi ya DC wameshindwa kufanya kazi yao kwani tukio hilo lilifanyika mita chache kutoka kambi yao.
“Maafisa hawa wa polisi hawakufika kwenye eneo hilo kwa wakati licha ya kuwa wako karibu,” Abel Njoroge alisema.
Mfanyibiashara huyo alivamiwa mwendo wa saa mbili usiku katika duka lake na kufariki alipofikishwa katika hospitali ya wilaya ya Bahati.
Njoroge amesema usalama umedorora sana kwenye eneo hilo wakati huu wa krisimasi.
Akidhibitisha haya, msimamizi wa wadi ya Bahati Newton Mwaura amesema eneo hilo linakabiliwa na ukosefu wa usalama. Amewataka polisi kuimarisha doria eneo hilo.
Mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri amekuwa akiwashutumu maafisa wa polisi kwa madai ya kuzembea kazini na kutoshirikiana na wananchi wanapohitajika.