Wito umetolewa kwa idara ya usalama nchini kuingilia kati hali tete ya usalama ambayo imeikumba eneo la Kisauni baada ya kundi la vijana wanaojulikana kama wakali kwanza kuvamia wakaazi waliokuwa wanatoka kazini hapo jana kwa mapanga.
Akiongea na mwanahabari huyu mkaazi ambaye gari lake liliharibiwa hapo jana na vijana hao Amina Omari amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kwa vijana hao kuwahangaisha wakaazi huku akidai kuwa maafisa wa polisi wanazembea kwa upande wao.
Huku hayo yakijiri idara ya polisi katika kaunti ya Mombasa imeahidi kulimaliza kikamilifu kundi hilo la wakali kwanza lenye makazi yake katika eneo bunge la Kisauni ambalo limekuwa likihusishwa na visa vya uhalifu kila kuchao.
Akiongea na mwanahabari huyu Kamanda mkuu wa polisi kaunti ya Mombasa Francis Wanjohi amesema kuwa makundi ya kihalifu ya 'Wakali Kwanza' na 'Wakali Wao' yanayowahangisha wakazi lazima yatakabiliwa kwa kutumia nguvu za sheria.
Wanjohi aidha amewataka wakazi wenye habari kuhusu vijana hao wenye umri wa chini ya miaka 20, kutoa habari kwa maafisa wa usalama.
Itakumbukwa kuwa hapo jana muda mchache tu baada ya Inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet kutoa onyo ya kuchipuka upya wa makundi haramu, wakali kwanza walivamia kijiji cha Kisauni na kupora umma na kuharibu mali yenye dhanmani huku watu watu wengine wakiuguza majeraha.