Wakaazi wengi wa jamii ya Turkana katika kaunti ndogo ya Rongai, jimbo la Nakuru, wana vitambulisho ambavyo vina kasoro, jambo ambalo huwaletea matatizo watoto wao wanaposailiwa ili kupata vitambulisho pindi wanapomaliza masomo ya kidato cha nne.
Akizungumza na mwandishi huyu kwa njia ya simu Jumatano, afisa anayesimamia usajili wa watu eneo la Rongai Emily Nyaga, amesema baadhi ya majina ya wazazi yaliyo kwenye vitambulisho, hayafanani na yale wanao hutumia shuleni ama wanayotumia kujisajili nayo jambo ambalo halipaswi.
“Tatizo hili limesababisha watoto wengi haswa walio wanafunzi kupata matatizo mengi wakati wa usajili mbalimbali kama wakati wa kusajiliwa katika mitihani ya kitaifa, na swala hili limesababisha watu wengi haswa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana kutopata vitambulisho,” Alisema Bi Nyaga.
Aliwachangamoto wazazi kutoka jamii hiyo, kutembelea afisi za usajili wa watu katika eneo hilo, ili waweze kutatua tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
Itazingatiwa kuwa katika siku za hivi majuzi, jamii hiyo imekuwa ikilalamika kuwa imebaguliwa katika eneo hilo haswa katika usajili wa kupata vitambulisho.
Ili kuondoa dhana hiyo, Bi Nyaga amewarai wazazi hao kushirikiana na afisi yake ili kuhakikisha wanapata vyeti hivyo muhimu.