Wakaazi na wafanyibiashara wa eneo la Kawauni katika kaunti ndogo ya Kangundo wamelalamikia ukosefu was kituo cha polisi katika eneo hilo kama sababu ya visa vya ukosefu was usalama kuongezeka.
Tukizungumza na baadhi ya wakaazi hawa siku ya Jumamosi walielezea kuwa tangu naibu wa chifu wa eneo hilo kustaafu miezi minane iliyopita hawajapata mwingine na hivyo visa vya ukosefu wa usalama kushuhudiwa kwa wingi.
Teresia Nzioka mchuuzi katika soko hilo alisema kuwa uuzaji wa pombe haramu ambao ulikuwa umpungua umerejea tena katika eneo hilo.
Aisha Nzioka alielezea kuwa wakaazi wamekuwa wakiishi kwa woga mwingi huku wakihofia kushambuliwa na wezi katika nyumba au duka zao.
"Tumeishi kwa woga mwingi kwa miezi minane tangu naibu wa chifu kustaafu kwani tangu wakati huo usalama wetu umekuwa mashakani," alisema Nzioka.
Wakaazi hawa walimtaka OCPD wa Kangundo Jane Kuria kuhakikisha wamejengewa kituo kidogo cha polisi.
Aidha walimwomba naibu wa kamishna wa Kangundo Samuel Njora kuhakikisha naibu wa chifu ameletwa katika eneo hilo ili kudhibiti usalama.