Wakaazi wa eneo bunge la Malindi katika Kaunti ya Kilifi wamelalamikia ukosefu wa usalama katika eneo hilo, baada ya kukamilika kwa uchaguzi mdogo siku ya Jumatatu.
Wakiongozwa na mwanaharakti wa vijana katika eneo hilo Salim Mohammed, wakaazi hao walisema kuwa wamekuwa wakiishi kwa hofu kufuatia tetesi kuwa baadhi ya vijana wanalenga kuzua vurugu na kuharibu usalama wa eneo hilo.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mohammed alisema baada ya uchaguzi mdogo wa eneo hilo kukamilika siku ya Jumatatu, usalama wa eneo hilo ulibadilika kwani maafisa waliokuwa wakishika doria waliondoka licha ya idara ya usalama katika eneo la Pwani kuahidi kuimarisha usalama hata baada ya uchaguzi huo mdogo.
Mohammed aliitaka idara ya usalama kutuma maafisa wake katika eneo hilo kukabiliana na baadhi ya vijana wanaojihami kwa mapanga na visu na kuhangaisha wakaazi.
Alisema kuwa hali hiyo huenda ikawa imechangiwa na uhasama wa viongozi wa kisiasa waliokuwa wakikita kambi katika eneo hilo kufanya kampeni zao za kisiasa.
“Tunaiomba idara ya usalama katika eneo la Pwani kuhakikisha kuwa inatuma maafisa wake kushika doria eneo la Malindi kwani tayari hofu imeanza kutanda kutokana na baadhi ya vijana kuanza kuwavamia wakaazi wasio kuwa na hatia,” alisema Mohammed.
Wakaazi hao walishinikiza idara hiyo kuwaimarishia usalama ili waweze kuishi kwa amani na kutekeleza shughuli zao za kila siku.