Karibu nyumba 200 katika maeneo ya Mbaruk viungani mwa mji wa Nakuru zimekumbwa na mafuriko baada ya mvua kubwa ambayo ilianza kunyesha siku ya Jumanne wiki hii.
Mkaazi mmoja, Stanley Kamau, alisema kwamba kuku wake wengi waliuawa na mafuriko hayo kutoka milima ya Dundori na Nyandarua.
Alisema kwamba vyoo vimejaa maji ya mafuriko, swala linalohatarisha afya yao zaidi.
Aidha, alisema baadhi ya familia hizo zimepoteza vyakula vingi.
“Kuku wangu wengi waliweza kusombwa na maji ya mafuriko, kwa sababu maji yanayotoka milima ya Dundori na ile ya Nyandarua yanatiririka kwa kasi, na kusomba kila kitu, hata vyakula vyetu shambani vimeharibiwa na mafuriko, na sasa huenda tukakumbwa na maradhi ya kipindupindu,” alisema Kamau.
Naye mkaazi David Njuhia mwenye umri wa miaka 88 alisema kilio chao cha maji hayo kutafutiwa njia ya kuondolewa pamoja na kujengwa kwa kuta za kukinga maji hakijatiliwa maanani.
“Tunaomba serikali ya kaunti ya Nakuru iweze kutusaidia maanake mkurupuko wa maradhi yanayosababishwa na maji chafu yanaweza kutukumba wakati wowote, tunaomba maji haya yaweze kutafutiwa njia mbadala, hata kama ni kuchimba mtaro au ukuta wa kuyazuia kasi ya maji,” alisema Mzee Njuhia.