Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wa eneo la Pwani na taifa nzima kwa jumla wameonywa kutopuuza uvimbe wowote unaotokeza miili mwao na badala yake kuvitembelea vituo vya matibabu ya saratani kujua hali zao.

Akiongea na wanahabari katika hospitali ya Coast Hospice mjini Mombasa siku ya Ijumaa, mwenyekiti wa kamati ya kitengo cha wagonjwa wa saratani katika hospitali hiyo Micheal Mutua ameeleza kuwa, ni vyema iwapo wakaazi watajua hali ya miili yao.

Amesema kuwa uvimbe mwingine katika mwili wa mwanadamu huwa hauna uchungu unapojitokeza mbali huenda ikawa ni dalili mojawapo ya ugonjwa wa saratani.

Mutua anayeugua saratani ya korodani ameongeza kuwa walioko mashambani wanaweza kujitokeza katika hospitali ili waweze kupata matibabu kwa haraka wanapoona uvimbe wowote katika mili yao kabla ya kuathiri afya zao.

“Ipo haja ya watu kutembelea vituo vya afya kwani mara nyingi watu wengi hukosa kufahamu kuwa wanaugua saratani na wanapoona uvumbe milini mwao wanadhani ni jambo la kawaida lakini uvimbe huo unawezakuwa chanjo za saratani mwilini,” alisema Mutua.

Aidha ameeleza kuwa wagonjwa wanaougua saratani wamekuwa na changamoto kutokana na ukosefu wa mashini ya radiotherapy kwani wagonjwa hulazimika kusafiri hadi jijini Nairobi katika hospitali kuu ya Kenyatta kwa matibabu hayo.

“Nadhani ingekuwa vyema kwa serikali kununua mashini za kutibu ugonjwa wa saratani kwani wagonjwa wengi hulazimika kutafuta matibabu katika hospitali kuu jijini Nairobi na inakuwa changamoto kwa wale wasio kuwa na uwezo wa kifedha kwa hivyo hilo ndilo ombi langu kwa serikali,” alieleza Mutua.