Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi eneo bunge la Bahati wameteta kuwa wanatozwa hongo kupata vitambulisho.

Baadhi ya wakaazi walioadhirika na swala hilo walisema kuwa kituo cha usajili cha Kiamaina kilicho Maili Sita, kimekithiri ufisadi ambapo inadaiwa kuwa kati ya shilingi 300 hadi 700 huitishwa ili wakaazi waweze kupata stakabadhi hiyo muhimu.

“Vijana wetu hawana vitambulisho, kwa sababu wanaitishwa shilingi mia nne,” Jackson Maina alisema.

“Ukipoteza kitambulisho inakuwa ni balaa kukipata upya, kwa sababu lazima utoe pesa ambazo hatujui na hatuambiwi ni za nini ilhali serikali inasema kitambulisho kuchukua ni bure. Tunaitishwa hadi mia saba, wengine mia tano,” Ngure Kamau alisema.

Walikuwa wakizungumza na aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA dakitari Abdul Noor Jumanne, ambaye alishtumu hatua ya kutoa vitambulisho kwa ubaguzi, hongo, au kuwataka makabila mengine kurudi walikozaliwa ili kutafuta vitambulisho.