Wakaazi wa Nakuru wameelezea furaha yao baada ya rufaa ya naibu rais William Ruto kukubalika kwenye mahakama ya ICC, katika uamuzi wa Ijumaa uliotolewa mahakamani hiyo iliyo mjini Hague, Uholanzi.
Mkaazi wa Nakuru Kibet Kuku, alisema japo ushindi huo wa ruto na mwanahabari Joshua arap sang ni wa muda, ni afueni kwake na Kenya ambayo inaponesha vidonda vya ghasia za baada ya uchaguzi 2o07/8.
“Ingekuwa si haki kwa mahakama ya ICC kutumia ushahidi wa watu ambao wamejiondoa kwenye kesi hiyo. Huo ni ushindi mkubwa kwa Ruto na Kenya, na sasa siasa za bonde la ufa zitakomaa,” alisema Kibet.
Micah Cheruiyot alisema: “Ombi letu kama wakenya ni kuona Ruto na Sang wakiwa huru, kwa sababu mahakama ya ICC imekuwa mahakama ya kukandamiza waafrika, sio kutafuta haki.”
“Tujiulize kama wakenya, je, ni Ruto na Sang peke yake walifanya Kenya yote kupigana? Kwa nini kesi za wanne kati ya Ocampo six zikatupiliwa mbali? Ni kwa sababu Ocampo alifanya uchunguzi hafifu, kuwabebesha mzigo wasiostahili. Ruto na Sang wawekwe huru pia, wachangie ukuaji wa Kenya kiuchumi,” alisema Susan Wambui.
Ruto na Sang’ walikuwa wamekata rufaa dhidi ya uamuzi wa majaji kumruhusu Bensouda kutumia taarifa za mashahidi watano waliojiondoa kwenye kesi dhidi yao.