Wakaazi wa kijiji cha Piave, kaunti ndogo ya Njoro Nakuru, wamelalamikia unyakuzi na uuzaji wa ardhi ya ekari nne ambayo ni mali ya umma.
Ardhi hiyo ambayo ilikuwa imetengewa shughuli za umma wakati wa ugavi wa ardhi ya kikundi cha Piave Nyakinyua Women wakati wa uongozi wa rais wa kwanza wa Kenya Mzee Jomo Kenyatta, sasa imewekwa nguzo na kuibua maswali mengi kuhusu ni nani haswa aliuza shamba hilo.
Wakaazi wa eneo hilo sasa wanaitolea changamoto tume ya ardhi nchini NLC kushirikiana na polisi kuchunguza na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.
Wakizungumza, wakaazi hao walisema kundi fulani la watu lilihusika katika ugavi wa ardhi hiyo wakisimamiwa na naibu chifu wa eneo hilo Roselyne Njeri.
“Jumanne tuliona watu fulani wakigawa hii ardhi kwa ekari mbili, wakiwa wamesimamiwa na chifu na hatujui iligawa ikauziwa nani,” mmoja wa wakaazi alisema.
Chifu huyo hata hivyo alikanusha madai hayo.