Serikali ya kaunti ya Nakuru imetakiwa kuipa hospitali ya Rajuera iliyoko kaunti ndogo ya Rongai vifaa vya matibabu ili wananchi waanze kupokea huduma.
Wakizungumza eneo hilo la Rajuera, wakaazi walisema kwamba, hospitali hiyo ilikamilika mwezi wa Janauari mwaka huu na inapaswa kupata vifaa hivyo ili kuweza kuanza kuwahudumia wakaazi.
Wakizungumza Ijumaa wakaazi hao wakiongozwa na Gladys Mwanzia walisema kwamba hospitali hiyo itakuwa ya manufaa kwa wakaazi haswa wa kutoka maeneo ya Mogoiwet, Lengenet, Naiswet, Kapsetek na Kampi ya Moto.
“Tunaomba serikali yetu ya kaunti ya Nakuru iweze kutuwekea vifaa vya kutumia katika hospitali hii kwani sisi hupitia shida kubwa wakati wa kutafuta matibabu,” Mwanzia alisema.
Naye Christopher Macharia alidokeza kuwa, huwa wanalazimika kusafiri hadi mjini Nakuru au Mogoiwet kupata matibabu.
“Ikiwa tutawekewa vifaa na dawa katika hospitali basi itakuwa rahisi na afueni kwetu kupata huduma bora kwa sababu huwa inatubidi twende hadi mjini Nakuru au hospitali ya Mogoiwet kutafuta matibabu na hutugharimu mno,” Macharia alisema.
MCA wa wadi ya Visoi Edward Gitau alisema wananchi wanapaswa kuwa na subira kwani mikakati imewekwa kuhakikisha kuwa hospitali hiyo inaanza kutoa huduma kwa wananchi.
“Nawaomba wananchi wawe na subira maanake tayari tumeweka mikakati na hivi karibuni hospitali hiyo itafunguliwa na kuanza kuwahudumia,” MCA huyo alisema.