Katika juhudi za kuimarisha usafi wa mazingira katika mji wa Mariakani, wakazi na wafanyibiashara katika mji huo wametahadharishwa dhidi ya kutupa taka ovyo barabarani.
Mwakilishi wa Wadi ya Mariakani Said Mwachenda alisema kuwa kumekuwa na utupaji ovyo wa taka mjini Mariakani hali ambayo imedunisha hadhi ya mji huo.
Akihutubia wakaazi katika warsha ya kuhifadhi mazingira bora baada ya kusambaza jumla ya mapipa tisa ya kutupia taka katika eneo hilo siku ya Ijumaa, Mwachenda alisema kuwa wakazi wanastahili kuzingatia usafi wa mazingira ili kujikinga na mkurupuko wa maradhi ambao mara nyingi huchangiwa na mazingira chafu.
“Kama nyinyi mmejitolea kikamilifu kujiepusha na mkurupuko wa maradhi ya kiafya ambayo huenda yakasababisha maafa, tafadhili tuweke mazingira yetu yakiwa safi. Hatua hiyo itafanikiwa iwapo tutashikina na kusafisha mji kwa kuweka taka zetu katika mapipa ya taka,” alisema Mwachenda.
Kiongozi huyo amesema kuwa mradi huo wa mazingira utapigiwa upato zaidi ili kuwahimiza wakaazi kutambua umuhimu wa kuhifadhi mazingira.