Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakaazi wa eneo bunge la Bahati kaunti ya Nakuru, sasa wametoa wito kwa idara ya ujenzi katika kaunti ya Nakuru, kuanzisha kampeni ya kuhakikisha kila ploti yenye nyumba za kukodisha inawekwa king’ora cha kukabiliana na mikasa ya moto na uhalifu kaunti hiyo.

Wakiongozwa na Josphine Waweru, wakaazi hao walisema kwamba uhalifu ambao umeongezeka Bahati utapungua iwapo kila ploti itawekwa kifaa cha kutahadharisha watu kuhusu jambo la dharura.

Walisema hayo baada ya wezi waliokuwa wamejihami kwa bunduki kuvamia ploti moja na kuwapora pesa na simu kati ya vifaa vingine vya kielektroniki katika wadi ya Kiamaina Jumapili usiku, mwezi mmoja tu baada ya mwanabiashara kuuawa wadi ya Bahati kwa kupigwa risasi.

“Tungetaka polisi washike doria zaidi, kwa sababu uhalifu umeongezeka. Lakini pia kila ploti iwe na king’ora, ili wahalifu wakija inakuwa kazi rahisi kujulisha wengine na polisi,” Josphine Waweru alisema.

Wito wake huo ulitiliwa mkazo na John Kariuki.

“Kila ploti sasa lazima iweke namna itakavyosaidia kukabiliana na uhalifu, kwa sababu nyumba kumi haifanyi kazi tena,” akasema.