Share news tips with us here at Hivisasa

Zoezi la usajili wa wapiga kura lilingia juma la pili kote nchini mnamo Jumatatu, huku wito wa wananchi kujitokeza kusajiliwa kwa wingi na kwa hiari kuwa wapiga kura ukizidi kutolewa na viongozi wa matabaka mbali mbali katika kaunti ya Kisumu.

Wa hivi punde kutoa wito huo ni Mwakilishi wa wadi ya Nyakach Kaskazini katika kaunti ya Kisumu Yona Koko.

Akizungumza mjini Katito mnamo Jumatatu, Koko alisema kuwa amezindua rasmi kampeini ya kuwahimiza wakaazi wa eneo hilo kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kama wapiga kura.

Alisema kuwa kupitia kampein hiyo, kundi moja la vijana limepewa jukumu la kuwaeleza wananchi vituo vya usajili wa wapiga kura vilipo.

Koko aliwahimiza wakaazi wa wadi hiyo kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kuwa wapiga kura.

“Kura ndio silaha pekee ya kuwachagua viongozi bora watakaoimarisha juhudi za maendeleo katika wadi hii, kaunti yetu na taifa letu,” alisema Koko.

Zoezi la usajili wa wapiga kura tayari limeingia juma la pili kote nchini.

Hata hivyo, idadi ya wananchi wanaojitokeza kusajiliwa ni ya chini mno.

Zoezi hilo la mwezi mmoja lililoanza tarehe 15 mwezi Februari, litakamilika tarehe 15 mwezi Machi.