OCPD wa Kisumu Christopher Mushimba, amewataka wakazi kujitokeza kuripoti visa vyovyote vya utovu wa usalama, hasa msimu huu wa likizo.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, Mushimba alisema kuwa polisi watahakikisha kuwa usalama unaimarishwa katika maeneo yote ya jiji la Kisumu na viunga vyake.
Aliwaomba wakazi kushirikiana na maafisa wa polisi ili kufanikisha lengo hilo.
“Kama alivyosema Rais Uhuru Kenyatta, usalama unaanza na mimi na wewe. Lazima kila mmoja awe tayari kuchangia katika vita dhidi ya uhalifu,” alisema Mushimba.
Mushimba alisema kuwa ni haki ya wananachi kupewa ulinzi na polisi, huku akisisitiza kuwa ni sharti wananchi wawe tayari kuwasaidia polisi kuwapa ulinzi.
Afisa huyo aliwataka wahudumu wa bodaboda, madereva, abira na wote wanaotumia barabara kuzingatia kanuni za trafiki ili kuzuia ajali.
“Yeyote atakayekiuka sheria za trafiki, ataadhibiwa vikali kisheria,” alisema Mushimba.
Mushimba alisema kuwa kila mmoja ana jukumu la kuwa mwangalifu barabarani, ili kuzuia ajali hasa ikizingatiwa kuwa ajali nyingi huripotiwa nchini wakati wa sherehe za krisimasi na mwaka mpya.