Mvua nyingi inapoendelea kunyesha katika baadhi ya maeneo ya nchi, wakazi wa eneo la Likoni katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kutumia neti ili kuzuia mbu nyakati za usiku na kuwasababishia maradhi ya malaria.
Wazazi walio na watoto wadogo pamoja na wanawake waja wazito walitahadharishwa dhidi ya kulala bila neti, huku wakiombwa kuzifuata kwenye hospitali za umma au kutoa ripoti katika afisi za idara ya afya ya umma katika Kaunti hiyo.
Kwenye mahojianao na afisa wa afya ya umma katika eneo la Bomu, Dkt Joel Oketch alisema ni bora zaidi wakazi kuzingatia ushauri wa maafisa wa afya ili kujiepusha na kupata maradhi yanayohusiana na mbu pamoja na maji ya mvua kama vile maradhi ya ngozi, kuharisha pamoja na malaria.
Alionya kuwa huenda kukashuhudiwa visa vya kuzaana kwa mbu ambazo kwa upande mwingine zitaongeza visa vya maradhi ya malaria kwa wakazi hususan wale ambao hawatatilia maanani wasia kutoka kwenye wizara na idara husika za masuala ya afya.
“Sharti sisi kama wakazi tuchukue jukumu kwenye mikono yetu na tufuate sheria na utaratibu, na ushauri ambao tunapewa hapa tuuweke maanani na tuutekeleze ili kuepusha familia na jamii kwa jumla kutoka kuambukizwa magonjwa ambayo yanaweza kudhibitiwa,” alisema daktari.