Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi katika eneo la Mgombezi LungaLunga, wamelalamikia ukosefu wa maji safi na barabara mbovu, hali waliyosema imepelekea ukosefu wa maendeleo katika eneo hilo.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatatu, wakazi hao walisema kuwa maji ambayo yanafaa kuwa hitaji la kimsingi yamekuwa adimu na kuzua hofu miongoni mwao.

Hamisi Mwaviriko, ambaye ni mzaliwa wa eneo hilo, alisema kuwa hajapata kuona kiongozi yeyote akishughulikia swala la barabara katika eneo hilo, tokea uwanja wa ndege wa eneo hilo kukomesha shughuli za kupokea ndege.

"Nimeishi huku kwa miaka ishirini sasa na barabara bado ni mbovu na hata maji safi hakuna. Wabunge tunaowachagua huenda huko bungeni kujinufaisha wao tu,” alisema Mwaviriko.

Matamshi yake yaliungwa mkono na Mama Aisha, ambaye alisema anashangazwa na viongozi wanaowachagua kuwawakilisha.

Alisema kuwa huwa wanamwona mbunge wao Khatib Mwashetani kunapokuwa na hafla pekee, tena kwa mbali.

Mwanajuma Salim, mkazi, alisema kuwa hawana imani tena na kiongozi yeyote atakayekuja na hoja ya kujenga barabara ama kuwachimbia visima, kwani wamegundua ni mbinu ya kujipatia kura.

"Huwa tunatembea masafa marefu kusaka maji ambayo mara nyingi huwa machafu,” alisema Salim.

Wakazi hao wamemtaka mbunge Mwashetani kuwajibika kabla ya mwaka ujao na kutimiza ahadi badala ya kuanza siasa za kukihama chama cha ODM.