Wakazi wa eneo la Mgombezi, huko LungaLunga, wamejitokeza kwa wingi kujisajili kama wapiga kura.
Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano, vijana walionekana kukumbatia zoezi hilo huku wakisema kuwa wameamua kufanya hivyo ndiposa wawe na uwezo wa kuwachagua viongozi wanaowataka.
"Tumeamua kujisajili ili ifikapo mwaka wa 2017, tuwe tuna nguvu na haki ya kuchagua mtu ambaye atajali maslahi yetu kama wakazi wa hapa Mgombezi,” alisema Ali Masoud, mkazi wa Mgombezi.
Matamshi yake yaliungwa mkono na mama Zawadi Mwanaisha, ambaye alisema kuwa mara nyingi akina mama wamekuwa wakipuuza mambo ya kura lakini kunapotokea majanga, hao ndio huumia sana.
"Wakati huu mpaka nasi tujitose ili tusibaki kulalamika kuwa hao waliochaguliwa hawafai. Viongozi wabaya na ambao hawana maendeleo hatuwataki tena," alisema Mwanaisha.
Mzee Khamis Mwaringo, alisema itakuwa mara yake ya pili kujisajili kwa sababu alikuwa akifanya kazi nje ya Mombasa kwa miaka mingi, na sasa amerudi nyumbani na lazima afanye hivyo ndiposa amchagua kiongozi amtakaye.
Zoezi la uasjili huko Mgombezi linaendelea vyema na wakazi wakiwemo akina mama na vijana, wanaendela kujisajili, huku zoezi hilo likiingia siku yake ya tatu.