Baadhi ya wakazi katika eneo la Kisauni katika Kaunti ya Mombasa wamempongeza Rais Uhuru Kenyatta kwa kumteua mbunge wa zamani wa eneo bunge la Mvita Najib Balala kuwa waziri wa utalii, hatua ambayo walisema itasadia kuinua hali ya sasa ya utalii eneo la Pwani.
Wakazi hao walidai kuwa Balala kwa wakati mmoja aliwahi kuhudumu kwenye wizara hiyo na alileta mabadiliko makubwa, na wanatarijia kuwa atafanya hivyo jinsi matarajio na matumaini ya wengi yalivyo hasa katika Kaunti sita za Pwani ambazo hushuhudia kuwasili kwa watalii mbalimbali kutoka nchi mtofauti ambao husaidia kuinua viwango vya uchumi.
Wakiongozwa na mzee Ramadhan Said, ambaye amekuwa akiwaongoza baadhi ya watalii katika baadhi ya sehemu za utalii kwenye jiji la Mombasa hasa kwenye mtaa wa kihistoria wa Free Town, Balala anauelewa na kufahamu vizuri sekta ya utalii pamoja na kuwa yeye ni mzawa wa Pwani atazingatia na kuendeleza utalii.
Ramadhan alisema kuwa ingekuwa vyems rais pia kuteua watu kwenye wizara kulingana na utaalam pamoja na tajiriba kwenye wizara husika kuliko kuweka baadhi ya watu kwenye nafasi hizo ambao mara nyingi huchangia kuporomoka na kudidimia kwa malengo ambayo wizara inadhamiria kufanikisha.
Mzee huyo aidha alisema hali hii huchangia mara nyingi kuzidi na kukithiri kwa ufisadi kwa sababu ya kukosa maarifa ya kuongoza idara au wizara husika.