Wakazi wa Mombasa wanamtaka kiongozi wa walio wengi katika bunge la kitaifa Aden Duale na mwenzake wa bunge la seneti Kipchumba Murkomen kujiuzulu baada ya kutajwa katika hati ya kiapo iliyowasilishwa na aliyekuwa waziri wa Ugatuzi Ann Waiguru.
Wakazi hao walisema siku ya Jumatano kuwa viongozi hao wanapaswa kuondoka mamlakani ili kutoa nafasi ya kuchunguzwa kuhusiana na sakata hiyo.
Salim Athuman, mkazi wa Mtwapa alisema kuwa kiwango cha ufisadi kimezidi mno hasa katika viongozi wa serikali, na kuongeza kuwa jambo hili linavunja moyo wananchi.
Aidha, wamemtaka mkurugenzi wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko kuiagiza idara ya upelelezi kuanzisha uchunguzi upya kwa wale waliohusishwa katika hati ya kiapo ya Waiguru ambayo alisema ilikuwa ya kutosha ili kuanzisha uchunguzi.
Duale na Murkomen pamoja msaidizi wa naibu rais William Ruto Farouk Kibet wametajwa katika hati ya kiapo ya waiguru kwenye kesi ya ufujaji wa shilingi milioni 791 za NYS.
Duale amekanusha madai yaliyotolewa na Waiguru ya kuwa anahusika katika sakata ya ufisadi.