Wakazi wa Mombasa wamepongeza hatua ya kukaguliwa kwa wahubiri wote kabla ya kuruhiswa kuhubiri katika shule za humu nchini.
Kwenye mahojiano na mwanahabri huyu siku ya Jumatano, wakazi hao, wa Kisauni wakiongozwa na Peter Kimani, walisema kuwa hatua hiyo itapunguza idadi ya vijana wanaojihusisha na misimamo mikali ya kidini nchini.
Aidha, wakazi hao wameitaka serikali kuzindua mbinu mbadala ya kukabiliana na visa vya ugaidi vinavyosababishwa na itikadi kali za kidini.
Kauli hii inajiri baada ya waziri wa elimu Fred Matiang’i, kusema kuwa wahubiri wote wanaozunguka katika shule za humu nchini sharti kupitia ukaguzi huo kabla kuruhusiwa kuhubiri katika shule.
Katika kongamano la wadau wa elimu, lililoandaliwa na baraza kuu la Waislamu nchini Supkem, na taasisi ya dini ya kiislamu IRE, wakiwemo walimu wa dini wanaoshikilia nyadhifa na wale waliostaafu, daktari Matiang’i alisema ni sharti uhuru wa kuabudu upewe hadhi inayostahili.
Matiangi alisema mtaala wa dini ya kiislamu uliozinduliwa na Supkem utawasaidia wanafunzi kuingiliana na tabia na mienendo inayokuza uvumilivu na heshima kwa binadamu.
Naibu katibu wa SUPKEM Hassan Ole Naado alisema mtaala huo umelenga kutoa elimu thabiti ili kuwakuza wanafunzi katika karne hii ya 21, kukidhi mahitaji yanayoambatana na mabadiliko bila kubadili ada na desturi zao.