Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi Mombasa wamepongeza kuteuliwa kwa mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Mombasa Mish Mboko katika kamati ya masuala ya bunge.

Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Jumatano, wakazi wa Likoni walisema kuwa hatua hiyo inaonyesha mfano mzuri na mwamko mpya kwa mwakilishi huyo hasa katika nyanja ya siasa na uongozi bora.

Hamisi Salim, mkazi, alimtaka kiongozi huyo kuwajibika pakubwa katika kuleta maendeleo kwa wananchi mashinani ikizingatiwa atakuwa akiwasilisha mrengo wa Cord katika kamati hiyo.

Siku ya Jumanne Mbunge wa Lunga Lunga Khatib Mwashetani aliondilewa katika kamati ya maswala ya bunge baada ya kuasi muungano wa Cord.

Katika barua kwa bunge la taifa siku ya Jumanne, Cord ilieleza kuliondoa jina la Mwashetani katika kamati inayowaleta pamoja wanachama 29 kutoka mirengo ya upinzani na serikali, huku nafasi yake ikipewa mwakilishi wa wanawake wa Kaunti ya Mombasa, Mishi Mboko.

Wiki iliyopita, mrengo wa Cord ulitishia kuwachukulia hatua wabunge waasi wa mrengu huo kwa kile walichokitaja kama kusalitiwa na wabunge hao, kutokana na hatua yao ya kufanya kazi na chama kipya cha JAP.

Tayari Cord imewaandikia barua wabunge hao huku ikiwataka kutoa sababu inayowafanya wasichukuliwe hatua kwa kufanya kazi na muungano wa Jubilee, licha ya kuwa walichaguliwa kwa vyeti vya Cord.

Kando na Mwashetani, wabunge wengine ambao huenda wakichakuliwa hatua na Cord ni pamoja na mbunge wa Kilifi Kaskazini Gideon Mung’aro, Peter Shehe wa Ganze, Salim Mustafa wa Kilifi Kusini na James Kamoti wa Rabai.