Huku raia kutoka kote nchini wakiendelea na zoezi la kujiandikisha kwenye maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao wa 2017, mshirikishi mkuu wa tume ya uchaguzi katika eneo la Pwani Gogo Nguma, amesema kuwa shughuli ya kujisajili bado inaendelea vizuri ila tu kuna idadi ndogo ya wakazi waliojitokeza.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Nguma aliwataka wakazi kujitokeza na kujiandikisha kama haki yao ya kikatiba, huku wakazi wakitaka kuongezwa kwa vituo vya kupiga kura.

Akiongea siku ya Alhamisi na mwandishi huyu, mshirikishi huyo aliwataka wanajamii, vyombo vya habari pamoja na watu binafsi kuchukua nafasi yao na kubandika vijikaratasi vyenye ujumbe wa upigaji kura, kwenye pahala pa kuonekana ili watu waweze kufanya uamuzi wa busara.

Aidha, baadhi ya maafisa ambao wanaendeleza zoezi hilo waliwataka waandishi wa habari kutangaza ujumbe huo kwa wenyeji.

Wakazi ambao waliongea na mwandishi huyu walisema kuwa baadhi ya wakazi huwa hawana nafasi ya kutembelea baadhi ya vituo kwa vile viko mbali, na kuitaka tume hiyo kujaribu kuweka vituo zaidi vya kusajili wapiga kura, badala ya kuendelea kutumia maeneo ya umma kama shule ambazo huwa mbali kwa baadhi ya raia.

“Wengine wetu hatuna wakati wa kupumzika na huwa tunatoka kazini tukiwa tumechelewa sana. Hivyo naomba tume ya uchaguzi nchini kubuni mbinu za ziada kama vile kutembea kila nyumba ili kufikia wale ambao hawana siku ya kupumzika,” alisema Laim Charo, mkazi.