Vijana na kina mama katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kuchukulia kilimo na ufugaji maanani ili kujinufaisha na kuimarisha hali yao ya uchumi.
Kwa kufanya hivyo, itakuwa rahisi kwa wakazi katika Kaunti ya Mombasa kuwa na njia mbadala ya kujipatia mapato na kuimarika badala ya kuwa na utegemezi wa pesa ya msaada kutoka kwa serikali.
Akiongea katika hafla moja ya kuwakabidhi makundi ya kina mama mbuzi jijini Mombasa, waziri wa kilimo katika Kaunti hiyo Antonny Njaramba alisema kuwa muda umefika kwa makundi mbali mbali kuundwa miongoni mwa jumuia za kina mama na vijana ili kufaidi katika miradi kama hiyo chini ya serikali ya Kaunti.
Njaramba aliwataka wale ambao walifaidi katika mradi huo kukaza bidii katika kuwafuga mbuzi hao, na kuimarisha riziki yao kupitia bidhaa ya maziwa itakayotokana na mbuzi hao.
Waziri huyo, alisema kuwa kila kundi ambalo limefaidi kutoka mradi huo litahitajika kuwa makini na kudokeza kuwa mradi huo unalenga kumfikia kila mkazi kwa kila uwakilishi wa wadi katika kaunti nzima ya Mombasa.
Hii ni mojawapo ya juhudi kutoka katika idara hiyo ya kilimo kwa niaba ya serikali ya kaunti kuhakikisha kuwa wakazi wanakuwa na mbinu za kupanua njia zao za kujipatia mapato na kuboresha hali ya maisha ya jamii zao.