Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi katika mtaa wa Mtongwe wameshtumu vikali mauaji ya kijana mmoja wa miaka 25 siku ya Jumatano asubuhi na afisaa mmoja anayedaiwa kuwa wa jeshi na kutaka haki kutendeka.

Kwenye mahojiano na baadhi ya wakazi na baadhi ya waliomjua kijana huyo, wakazi hao walisema kuwa kijana huyo alikuwa mwenye akili punguani na alipigwa bila kuzingatia hali yake ya afya na kuitaka idara ya polisi kuchukua hatua ya haraka ili kuchunguza mauaji hayo.

Silas Karuma, ambaye ni mkazi wa eneo la Vijiweni na ambaye ni mchuuzi wa bidhaa za mali mali katika maeneo mbali mbali eneo bunge hilo alisema kuwa kijana huyo amejua binafsi kama miezi miwili na alikuwa akimwona akitembea kila mahali na hana akili timamu.

Naye Mwanaidi Chewa alishtumu mauaji hayo akishangaa ni vipi afisaa huyo angeweza kumuua mwendawazimu huyo hata kama alikosa kiasi gani na kutaka hatua ya haraka kuchukuliwa dhidi ya mwanajeshi huyo aliyehusika.

Mwenda zake Mwema Ndolo anasemekana kuaga dunia kwa kupigwa risasi na afisaa wa jeshi karibu na shule ya msingi ya Dona-Linda kwa madai kuwa alikuwa anawapura mawe wanafunzi wakienda shule, ambapo mwanajeshi aliyekuwa kwenye gari alifyatua risasi na kumuua papo hapo.

Hata hivyo afisaa mkuu wa polisi eneo la Likoni Willy Simba amewahakikishia wakazi kuwa kisa hicho kinaendelea kufanyiwa uchunguzi ili sheria ifuatwe.