Mkuu wa kaunti ndogo ya Nakuru Kaskazini Githinji Ithae, amewataka wakazi wa eneo hilo kuhudhuria mikutano ili kujumuika na maafisa husika katika majadiliano kuhusu maswala, maoni na mapendekezo ya eneo hilo.
Akiwahutubia wakazi katika uwanja wa michezo wa Bahati wakati wa maadhimisho ya siku ya Jamuhuri siku ya Jumamosi, Bw Ithae alisema wakazi huchangia pakubwa wakati wa mikutano kwani wana fursa ya kukosoa utendakazi wa idara za serikali ambazo zimezembea kazini.
“Ningependa muwe mkihudhuria mikutano muhimu ambazo hufanywa na viongozi ili muweze kuwasilisha mapendekezo na shida ambazo zinawakumba kule mashinani. Tuko hapa ili kuwahudumia.” alisema Ithae.
Aliongeza, “Kumbukeni kuwa nyinyi ndio macho ya serikali. Mnapoonyesha ushirikiano, tutaweza kutatua baadhi ya matatizo makuu ambayo yanatukumba.”
Aidha, amewetaka wakazi wazidi kushirikiana na vyombo vya usalama katika vita dhidi ya pombe haramu, na pia uhalifu kwa njia ya kuwasiliana na ofisi za utawala.
Wakati huo huo, Ithae alivionya baadhi ya vyombo vya habari vya humu nchini dhidi ya kuiripoti matukio bila udhibitisho.
Alivitaka vyombo hivyo kuwajibika kwa kupata ukweli wa matukio kabla ya kuyapeperusha hewani.