Mwakilishi wa wadi ya Nyamira mjini Robert Ongwano amewahimiza wakazi wa kaunti ya Nyamira kuhifadhi maji ya mvua.
Akihutubia wanakijiji wa Bomondo siku ya Jumatatu alipokuwa akikagua miradi mbalimbali ya maendeleo, mwakilishi wadi huyo alisema kuwa itakuwa vizuri iwapo wakazi watachukua hatua ya kuhifadhi maji ya mvua kwa minajili yakujiandaa kwa msimu wa ukame unaotarajiwa mwaka ujao.
"Nawaomba wakazi wa kaunti hii kuhifadhi maji kwa wingi hasa msimu huu wa mvua kwa matumizi ya baadaye wakati wa msimu wa kiangazi,” alisema Ongwano.
Ongwano pia aliwahimiza wakazi kupanda miti na mboga kama njia moja ya kuimarisha mapato yao ya kila siku.
Mwakilishi huyo aidha aliwataka wakazi hao kuwa na subira kwa kuwa ukarabati wa barabara zilizoko katika hali mbaya ulisitishwa kwasababu ya mvua inayoendelea kunyesha.
"Nawasihi wananchi kupanda miti na mboga katika msimu huu wa mvua ili kuimarisha mapato yenu ya kila siku. Vilevile nawaomba muwe na subira kwa kuwa tutarejelea ukarabati wa barabara pindi tu mvua itakapopungua,” alisema Ongwano.