Baadhi ya wakazi wa kaunti ya Nyamira wamejitokeza kulalamikia vikali hali ya kuziba kwa mabomba ya maji taka katika eneo hilo.
Wakihutubia wanahabari mjini Nyamira, wakazi hao hasa wafanyibiashara wamesema kwamba hali ya mabomba ya maji taka kuendelea kuziba katika eneo hilo hasa kwenye msimu huu wa mvua inawaweka kwenye hatari yakuambukizwa magonjwa mbalimbali.
"Hali hii ya mabomba ya maji taka kuendelea kuziba katika mitaa ya humu Nyamira inatuweka kwenya hatari yakuambukizwa magonjwa hasa kipindupindu na malaria kwa maana mbu wanaweza pata mahala pakuzalia mayai," alisema msemaji wa wanabiashara hao Gilbert Ong'ondi.
Ong'ondi aidha aliongeza kwa kuhimiza waziri wa mazingira maji na mali asili katika kaunti hiyo Kepha Osoro kuweka mikakati yakuhakikisha kuwa mabomba hayo yanazibuliwa kwa haraka huku wakitishia kuandamana iwapo hilo halito tekelezwa kwa wiki moja ijayo.
"Sisi hulipa ushuru kwa serikali ya kaunti hii natunashangazwa na ni kwa nini serikali ya kaunti hii kupitia kwa wizara ya mazingira maji na mali asili haiwezi kuweka mikakati yakuzibua mabomba haya na ndio maana tunaipa wizara husika wiki moja kuchukua hatua la sivyo tuandamane," aliongezea Ong'ondi.